Yanga mmeibeba Tanzania, pambaneni kwa jasho

0
553

Yanga SC, moja ya vilabu vikongwe barani Afrika, ipo katika mawindo ya kutafuta heshima kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) leo hii, ikiwa na kibarua ugenini dhidi ya MC Alger. Nawakumbusha Yanga tu kuwa mmeibeba Tanzania, pambaneni.

Ushiriki wa Yanga SC katika mashindano haya ni fursa ya kuonyesha uwezo wao na hatua muhimu kwa maendeleo ya soka nchini Tanzania. Ingawa walianza vibaya kwa kufungwa 2-0 na Al Hilal nyumbani, matumaini ya kufanya vizuri ni makubwa.

Timu hii kongwe, yenye historia ya kuanzia mwaka 1935, imekuwa na mafanikio makubwa katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Yanga ndio timu iliyochukua ubingwa mara nyingi zaidi kulinganisha na timu yoyote na ina mashabiki wengi si tu nchini, bali pia katika Afrika Mashariki.

Katika miaka ya hivi karibuni, Yanga SC imewekeza fedha nyingi katika kuboresha kikosi chake. Usajili wa wachezaji wenye vipaji na kuajiri benchi la ufundi lenye weledi umekuwa chachu ya mafanikio yao, ikiwemo kufika robo fainali ya Klabu Bingwa Barani Afrika msimu uliopita.

Kushiriki kwa Yanga SC msimu huu kuna hamasisha matarajio makubwa kutoka kwa mashabiki na wadau wa soka. Hata MC Alger sasa inaitazama Yanga kama moja ya timu kubwa barani Afrika.

Kikosi cha Yanga kinaaminika kutokana na usajili wa wachezaji wa kimataifa wenye uwezo mzuri. Ushirikiano wa wachezaji hawa na wale wa muda mrefu ni silaha muhimu kwa mafanikio yao.

Mashabiki wa Yanga, maarufu kama Wananchi, wanaendelea kutoa sapoti kubwa, ambayo inazidisha morali ya wachezaji.

Tafakuri Angavu inahitimisha kwa kusema: Kushiriki kwa Yanga SC katika Klabu Bingwa Afrika ni nafasi ya kuonyesha uwezo barani na kukuza heshima ya soka la Tanzania. Uwekezaji uliofanyika na sapoti ya mashabiki inaonesha matumaini makubwa.

Tunawatakia ushindi katika mchezo wenu wa leo dhidi ya MC Alger.
Mungu ibariki Yanga Afrika.
Mungu ibariki Tanzania.