Wizara ya Madini yapewa mtihani ukusanyaji mapato

0
233

Rais Dkt. John Magufuli amemuapisha Profesa Shukrani Manya kuwa Naibu Waziri wa Madini baada ya kumteua mapema hii leo kuwa Mbunge na Naibu Waziri wa Madini.

Akizungumza mara baada ya kumuapisha Profesa Manya Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, Rais Magufuli amempongeza kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo na kumtaka kwenda kuchapa kazi.

Amesema ameamua kumteua Profesa Manya sababu ana taaluma inayohusu masuala ya madini na ana imani atafanya vizuri akiwa katika nafasi hiyo.

Rais Magufuli amewataka Watendaji wa wizara ya Madini kujipanga vizuri ili kuhakikisha mapato yatokanayo na sekta ya madini yanaongezeka.

Amesema kuwa anataka kuona sekta ya madini inaongoza katika kuchangia pato la Taifa na kuwanufaisha wale wote wanaojishughulisha na sekta hiyo.

Kabla ya uteuzi huo, Profesa Manya alikuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Tanzania.