Wizara ya afya yalaani vitendo vya ukatili kwa watoto nchini.

0
1142

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inalaani na kukemea vikali vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinavyoendelea kujitokeza nchini.

Taarifa iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano cha wizara imesema kuwa vitendo hivyo vinafanywa na kuhusisha ndugu na walezi wa karibu wa watoto, hivyo kuzua hofu kubwa katika jamii kwani vitendo hivyo  vinaathiri malezi na makuzi ya awali ya watoto.

Taarifa hiyo imeelezea tukio liloripotiwa kuhusu mwalimu wa shule moja  ya msingi jijini Dodoma ambaye anatuhumiwa kumfungia mtoto mdogo ndani ya kabati kwa takribani miaezi mitano  na kusababisha afya ya mtoto huyo kudhohofika.

Pia Mwalimu huyo anatuhumiwa kumfanyia vitendo vya ukatili mama mzazi wa mtoto  huyo kwa kumpiga na kumsababishia maumivu mwilini yaliyosababisha  binti huyo na mtoto wake kulazwa.

Wizara inawapongeza wanajamii wote walioibua tukio hilo na kuwezesha Jeshi la Polisi kumkamata mtuhumiwa kwa ajili ya uchunguzi ili Sheria ichukue mkondo wake.

Matukio ya ukatili kwa watoto  yanarudisha nyuma jitihada za Serikali za kulinda na kuendeleza haki na ustawi wa watoto katika ngazi ya familia ambayo ndio kitovu cha jamii.

Hata hivyo wizara inatoa wito  kwa jamii  kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii ili kuepuka makosa ya kisheria yanayoweza kutokea kwa kusambaza, kuchapisha na kupiga picha za watoto ambao ni wahanga wa ukatili na kuziweka wazi kinyume na Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009.