Wilaya zatakiwa kufanya tathmini ya mali zake

0
2673

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa wilaya nchini kushirikiana na madiwani katika halmashauri zao kufanya tathmini ya mali zote zinazomilikwa na halmashauri vikiwemo vibanda vya biashara ili kujiridhisha kama viwango vya kodi vinavyotozwa vinalingana na hali halisi ya uchumi kwa sasa.

Amesema kuwa mbali na tathmini hiyo kuwawezesha kufahamu viwango vinavyotozwa, pia itazisaidia halmashauri kubaini watu wa kati ambao wanawatoza wafanyabiashara fedha nyingi na kuilipa halmashauri fedha kidogo, jambo linalochangia kuikosesha serikali mapato.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya mji wa Nzega na wa Halmashauri ya wilaya ya Nzega pamoja na madiwani, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi wilayani Nzega mkoani Tabora.

Ametoa agizo hilo baada ya Mbunge wa Nzega Mjini, Husein Bashe kuomba serikali iingilie kati mgogoro uliopo baina ya halmashauri na wafanyabiashara kuhusu mradi wa vibanda vya biashara katika eneo la Soko Kuu la Nzega ambavyo vimejengwa na wafanyabiashara katika ardhi ya halmashauri kwa makubaliano ya kulipa kodi.