Shirika la Afya Duniani (WHO) limesitisha majaribio ya dawa aina ya Hydroxychloroquine kwa wagonjwa wa corona, baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa dawa hiyo ambayo imekuwa ikitumika kwa ajili ya kutibu malaria inaongeza vifo miongoni mwa wagonjwa wa corona.
Majaribio hayo yalikuwa yakifanywa kwa ushirikiano na wanasayansi kutoka mataifa mbalimbali duniani, lengo likiwa ni kupata tiba dhidi ya virusi vya corona.
Wiki iliyopita wanasayansi wa Marekani na Russia walisema kuwa dawa hiyo aina ya Hydroxychloroquine na dawa nyingine za aina hiyo zinaweza kuharakisha kasi ya mapigo ya moyo na kuzidisha hatari ya kufariki dunia kwa mgonjwa wa corona.
Kwa mujibu wa Wanasayansi hao, hawakubaini ufanisi wowote wa dawa hiyo katika kutibu wagonjwa wa corona.
Mtendaji Mkuu wa WHO, Dkt Tedros Ghebreyesus amesema shirika hilo kwa sasa linachunguza data za usalama wa dawa hizo.