Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wangi Yi, kesho anatarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.
Akizungumza na Waandishi wa Habari wilayajni Chato mkoani Geita, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa, Waziri Yi atawasili
katika uwanja wa ndege wa Chato majira ya jioni na kuanza ziara yake.
Profesa Kabudi amesema kuwa, atakapokuwa nchini Waziri Yi atafanya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzindua Chuo cha Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA) cha wilaya ya Chato.
“Hapo kesho mara baada ya kuwasili hapa Chato, Waziri Yi atazindua Chuo cha VETA cha Wilaya ya Chato ambacho kimejengwa kwa fedha za Watanzania na ukumbi mmoja ambapo umepewa jina lake,” amesema Profesa Kabudi.
“Sababu ya kumuomba afungue chuo hicho ni utamaduni wetu wa kumpa heshima mgeni anapokuja hapa kwetu, sambamba na kutambua elimu ya mafunzo na ufundi stadi ilivyopiga hatua huko nchini China,” amesisitiza Profesa Kabudi.
Kwa mijibu wa Profesa Kabudi, Serikali ya China inatarajia kujenga Chuo cha VETA mkoani Kagera, ikiwa ni namna ya kufikia lengo la Serikali kujenga VETA kila wilaya hapa nchini.
Ametaja shughuli zingine zitakazofanywa na Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa China, kuwa ni kufanya mazungumzo na Rais Dkt John Magufuli.
Profesa Kabudi amesema kuwa ziara ya Wangi Yi nchini imesaidia kuwataarifu watu wa China kuhusu hifadhi tano mpya nchini ikiwemo ya Burigi-Chato.