Waziri Ummy : Wananchi fanyeni uchunguzi wa awali kwa kupima saratani ya matiti

0
204

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amewataka wananchi kufanya uchunguzi wa awali wa kupima Saratani ya Matiti ili kujua hali zao na kupata matibabu mapema kwa wenye changamoto hiyo.

Waziri Ummy ameyasema hayo wakati akimwakilisha Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango kwenye Maadhimisho ya Mwezi wa Saratani ya Matiti yaliyofanyika katika viwanja vya Taasisi ya Saratani Ocean Road Jijini Dar es Salaam.

“Wataalamu wanatueleza kwamba mtu anaweza kujichunguza mwenyewe na akiona mabadiliko ya uvimbe katika titi, basi anashauriwa kuwahi katika kituo cha kutolea huduma za Afya kwa uchunguzi zaidi”. – Amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amesema Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya wa Saratani takribani Elfu Arobaini na Mbili (42,000) kila Mwaka huku asilimia 38 kati ya hao ndio wanafika katika vituo vya kutolea huduma za Afya.

“Wakati Tanzania tunakadiriwa kuwa na wagoniwa wapya wa Saratani takribani Elfu Arobaini na Mbili (42,000) kila Mwaka, wagonjwa asilimia 38 tu ndio wanafika Hospitali, maana yake katika kila wagonjwa 100 wa Saratani, wagonjwa 38 tu ndio wanafika katika vituo vya kutolea huduma za Afya”. Amesema Waziri Ummy

Pia, Waziri Ummy amesema taarifa ya mwaka 2022/2023, inaonesha kuwa Taasisi ya Saratani Ocean Road ilihudumia wagonjwa wapya takriban 8,779 na asilimia 13 ya wagonjwa hao sawa na wagonjwa 1,141 walikuwa na Saratani ya Matiti.