Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya imefanya uchunguzi wa ugonjwa uliolipuka kusini mwa Tanzania na kuchukua sampuli za ugonjwa huku majibu yakionyesha kuwa sio ugonjwa wa Ebola, Maburg wala UVIKO-19.
Waziri Ummy amesema hayo alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha 22 cha kisekta cha Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kilichofanyika Jijini Arusha .
“Kuna Mlipuko wa ugonjwa usiojulikana Kusini mwa Tanzania (Lindi) na tayari timu ya Watalaam wetu iko huko. Sampuli zimechukuliwa kutoka kwa wagonjwa na kuonyesha kuwa siyo Ugonjwa wa Ebola, Maburg wala UVIKO-19”
Waziri Ummy amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imekubali ombi kutoka Shirika la Afya Duniani na kutoka Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Magonjwa (CDC) kutoka Serikali ya Marekani ili kuongeza nguvu kwenye timu ya wataalam katika kubaini ugonjwa huo.