Waziri Ndalichako: Wazazi pelekeni watoto shule

0
179

Waziri wa Elimu,, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amewataka wazazi na walezi kuwapeleka shule watoto wenye umri wa kwenda shule.

Akizungumza mkoani Katavi leo wakati akizindua Ofisi ya Uthibiti Ubora wa Shule, Waziri Ndalichako amesema hakuna sababu yeyote itakayozuia mtoto kuanza shule kwani serikali imeshatoa ada na michango yote iliyokuwa kikwazo kwa wazazi kupeleka watoto shule. “Serikali ya awamu ya Tano ilipoingia madarakani iliondoa ada na michango yote iliyokuwa kero kwa wazazi na walezi ambayo ilipelekea watoto wengi kushindwa kuandikishwa lakini leo changamoto hizo hazipo hivyo hakuna sababu za kushindwa kuwapeleka shule,” amesisitiza Waziri Ndalichako.

Profesa Ndaliichako amesema serikali ilichukua jukumu la kulipa ada hizo na michango yote ili kuhakikisha hakuna mtoto yeyote wa kitanzania anabaki nyumbani bila kupata elimu msingi ambayo ni muhimu.

Aidha, Waziri Ndalichako amewataka wazazi wenye watoto wenye mahitaji maalum kutosita kuwapeleka shule kwani serikali ilishaboresha na kujenga miundombinu rafiki kwa ajili yao.

Ndalichako amesema mbali ya kuweka miundombinu rafiki serikali pia imenunua vifaa saidizi na kuvisambaza shule kwa ajili kuwezesha wanafunzi wenye mahitaji maalumu kusoma bila changamoto zozote.

Wakati huo huo, Profesa Ndalichako amewaagiza wathibiti ubora wa shule kuhakikisha shule zote zenye changamoto ndogondogo kusaidiwa kuwezesha shule hizo kuanza mara moja kudahili wanafunzi kwa ajili ya kidato cha kwanza. “Wathibiti ubora wa Shule, kesho shule zinafunguliwa nawaagiza kushirikiana na shule zote zilizoleta maombi kwa ajili ya usajili na kukutwa na makosa madogo mzisaidie ziweze kusajiliwa bila kujali ni za serikali ama binafsi” amesisitiza Profesa Ndalichako.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknojia anaendelea na ziara yake ya siku mbili mkoani Katavi ambapo leo atapokea majengo kwa ajili ya tawi la Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine