Waziri Ndaki ataka kupuuzwa kwa uzushi wa wingi wa mayai kutoka nje ya Nchi

0
206

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka Watanzania kupuuza uzushi uliojitokeza kutokana na kusambazwa kwa ujumbe wenye taarifa za kupotosha kuhusu kuingizwa kwa mayai nchini kutokea nchi jirani na kusababisha soko la mayai yanayozalishwa nchini kushuka bei kufikia shilingi 4,000 kwa trei.

Akizungumza mkoani Dodoma, Waziri Ndaki amesema baada ya kuona ujumbe huo Juni 15 mwaka wizara ilifanya uchunguzi kwenye makao makuu ya mikoa yote 26 nchini na baadhi ya wilaya ili kujiridhisha juu ya upatikanaji wa mayai, bei ya trei ya mayai na soko lake kwa ujumla.

Akizungumzia matokeo ya uchunguzi huo, Waziri Ndaki amesema mayai yanayozalishwa nchini ni kidogo kwa sababu ya uhaba wa vifaranga wa kuku wa mayai na tatizo la uhaba wa vifaranga limekuwepo tangu mwaka 2020 kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID19 duniani uliosababisha uingizaji nchini wa vifaranga wa kuku kupungua sana.

Amesema taarifa zilizosambazwa ni uzushi mtupu na hazina ukweli wowote kutokana na kwamba serikali ilishazuia uingizwaji wa kuku na mazao yake kutokana na uwepo wa tishio la ugonjwa wa mafua makali ya ndege duniani.