Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameliagiza Shirika la Posta Tanzania kuwa wabunifu katika kutangaza shughuli wanazozifanya ili huduma zao ziweze kuleta tija kwa Wananchi.
Waziri Nape ameyasema hayo jijini Arusha wakati wa hafla ya uzinduzi wa Biashara ya Bima ya Shirika la Posta (Posta Insurance Broker).
“Kuanzishwa kwa huduma au Biashara ni jambo moja lakini kuwafikia walengwa ndio jambo la msingi, hivyo nawaelekeza Posta Ili muweze kufikia malengo nguvu kubwa inahitajika katika kuitangaza biashara yenu katika vyombo vya habari, na kuwafuata walengwa walipo kupitia njia mbalimbali ikiwemo mikutano na semina mbalimbali ili kuwapa elimu ya umuhimu wa bima hasa wale wakulima wa vijijini ambao ofisi nyingi za Posta ndiko ziliko,” Amesema Waziri Nape.
Pia amelipongeza Shirika la Posta kwa Ubunifu walioufanya wa kuanzisha Bima hiyo kwani ni ishara tosha ya kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha Watanzania wengi wanapata fursa ya kuunganishwa na mifumo rasmi ya watoa huduma mbalimbali mahali pamoja.