Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amesema suala la kukatika kwa umeme mara kwa mara katika mikoa ya Lindi na Mtwara linasababisha mitambo ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kushindwa kufanya kazi ipasavyo, hivyo suala hilo linapaswa kushugulikiwa haraka.
Waziri Mwakyembe ameyasema hayo alipokua katika ziara ya kukagua mitambo ya TBC iliyopo Kipihe mkoani Lindi ambapo amesema suala hilo ni la kisera hivyo ataliwasilisha Wizara ya Nishati ili litafutiwe ufumbuzi wa kudumu.
“Maeneo ya kimkakati hayapaswi kukosa umeme wa uhakika, eneo hili la Kipihe ni mojawapo ya maeneo ya kimakati ambayo yanasaidia shirika letu la utangazaji TBC kutoa habari kwa wananchi wa mikoa ya kusini hivyo umeme lazima uwe wa uhakika utakaowezesha mitambo hiyo kufanya kazi kwa ufanisi na muda wote,” amesema Mwakyembe.
Ameongeza kuwa TBC ni chombo cha umma ambacho kina wajibu wa kuelezea wananchi nini Serikali imefanya katika nchi na inatarajia kufanya nini katika siku zijazo hivyo changamoto yoyote inayojitokeza katika chombo hicho ni lazima itafutiwe ufumbuzi wa haraka.
Kwa upande wake mhandisi wa shirika hilo, Upendo Mbele amesema kwamba usikivu wa shirika hilo umeendelea kuimarika ambapo maeneo mengi yanafikiwa kwa ubora unaotakiwa kufuatiwa kufungwa mitambo ya kisasa katika mkoa huo.
Mbele ameongeza kuwa ndani ya wiki mbili zijazo eneo la Kipihe litawekewa jenereta ambalo litasaidia pale umeme unapokatika mitambo isizimike ambayo inasababisha matangazo ya redio kukatika, huku akieleza kuwa Mwaka wa fedha 2020/2021 TBC imetenga fedha kwa ajili ya kuimarisha studio ya Kanda ya Kati, Dodoma.