Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema, sekta ya mifugo bado haijaleta tija katika pato la Taifa licha ya Tanzania kushika nafasi ya pili kwa kuwa na mifugo wengi Barani Afrika kwa hivi sasa.
Akifungua mkutano wa wadau wa sekta ya mifugo hapa nchini, Waziri Mkuu amesema, sekta ya mifugo haifanyi vizuri kutokana na wafugaji wengi kutunza mifugo yao kienyeji, na hivyo kushusha thamani ya mazao ya mifugo.
Waziri Mkuu amesema, wafugaji wengi wamekuwa wakifuga kwa njia ambazo hazina tija kwenye mazo ya mifugo hali inayofanya mazao ya mifugo kukosa thamani inayotakiwa kwa wanunuzi wa nyama, maziwa na ngozi.
Aidha ameitaka wizara ya mifugo kuangalia namna bora ya kuongeza thamani katika mazao ya mifugo na kubadili mtindo wa ufugaji kutoka mfumo wa sasa wa kufuga kienyeji na kufuga kisasa ili kuongeza thamani ya mazao ya mifugo.
Waziri Mkuu pia amesisitiza kuwa masoko ya nyama yapo kila kona ya dunia lakini ubora wa nyama ndio jambo muhimu la kuzingatia kabla ya kuamua kuiza nyama hiyo nje ya nchi.
Hata hivyo Majaliwa ameiagiza wizara ya mifugo kuangalia maeneo ya ranchi za Taifa ambayo hayana mifugo kuruhusiwa kutumika na wafugaji ili kuongeza wigo wa machungio ya mifugo hapa nchini.