Waziri Mkuu : Jiepusheni na Rushwa

0
243

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watendaji wa Serikali kujiepusha na vitendo vya rushwa, pamoja na kuepuka urasimu usiokuwa wa lazima katika kuwahudumia Wawekezaji.
 
Waziri Mkuu Majaliwa, pia ameziagiza wizara na taasisi zote zinazohudumia Wawekezaji kuhakikisha wanawawezesha katika maeneo walipo kwa kutoa huduma na taarifa muhimu kwa wakati.
 
Agizo hilo limetolewa Bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu Majaliwa wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022.
 
Amesema tarehe 6 mwezi huu alipokuwa akiwaapisha Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Wakuu wa baadhi ya Taasisi za Serikali Ikulu jijini Dar es salaam, Rais Samia Suluhu Hassan alisisitiza masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwekezaji na vibali vya kazi.
 
“Mheshimiwa Rais aliielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu kuimarisha huduma za pamoja (One Stop Centre), kushughulikia malalamiko kuhusu kodi, kuondoa vikwazo katika uwekezaji, kuhamasisha uwekezaji kupitia mazungumzo, ushawishi, kudhibiti rushwa na kuondoa urasimu kwenye maombi ya vibali vya kazi,” amesema Waziri Mkuu.
 
Amesema maelekezo hayo ya Rais Samia Suluhu Hassan yenye kujali maslahi ya Taifa yalikuwa ni pamoja na uamuzi wake wa kuunda rasmi wizara ya Uwekezaji chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa lengo la kuhakikisha wizara hiyo inasimamia kikamilifu masuala ya uwekezaji.
 
Amesema tayari maelekezo hayo yameanza kutekelezwa kwa kuandaa muundo wa wizara ambao utaainisha majukumu na mgawanyo wa Idara na Taasisi zitakazokuwa chini ya wizara hiyo.