Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa vitendo vya udokozi wa mali ya umma havitavumiliwa na serikali na hivyo kuwataka watumishi wa umma kuwa waadilifu na waaminifu wanapotekeleza majukumu yao.
Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani humo.
“Serikali haitamvumilia mtumishi wa umma ambaye si muadilifu, mvivu na mla rushwa, hivyo ni lazima watumishi wawajibike na ambao watashindwa kutekeleza majukumu yao watapa shida kwenye Serikali hii, hakuna mchezo kwenye serikali hii, watumishi wa umma wanapaswa kulitambua hili” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma wahakikishe wanapanga ratiba ya kwenda kuwatembelea wananchi hususani wanaoishi katika maeneo ya vijijini na kushirikiana nao katika kutatua kero mbalimbali zinazowakabili na si kukaa ofisini.
Ameongeza kuwa sio kila mtumishi kwenye idara yake anapaswa kwenda kwa wananchi, kama ana siku tano za kufanyakazi kwa wiki basi siku tatu azitumie kwenda kwa wananchi kutatua changamoto zao na kama ana siku sita, siku nne azitumie kwa kufanya jambo hilo.
Waziri Mkuu Majaliwa pia amewasisitiza watumishi wa umma kuzingatia itifaki, mipaka ya madaraka yao pamoja na kuheshimu viongozi na kwamba hata kama ni mkuu wa idara pia anapaswa kumheshimu mtumishi aliyekuwa chini yake.
Awali, Spika wa Bunge Job Ndugai ambaye ni Mbunge wa jimbo la Kongwa aliishukuru serikali kwa kutatua kero mbalimbali ikiwemo changamoto ya ukosefu wa maji pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mbande hadi Kongwa ambapo aliomba ujenzi huo uendelee hadi Mpwapwa.