Waziri Mkuu ataka nyumba za ibada zisigeuzwe majukwaa ya siasa

0
236

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa taasisi za kidini nchini  kujiepusha kutumia nyumba za ibada kama majukwaa ya siasa.
 
Badala yake Waziri Mkuu Majaliwa amezitaka taasisi hizo kuendelea kushirikiana na Serikali katika kujenga Taifa la watu wenye hofu ya Mungu, heshima, upendo na wenye kudumisha amani na utulivu.
 
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa wito huo mkoani Pwani wakati wa hafla ya uzinduzi wa msikiti wa Jamiu Assaliheen uliojengwa na taasisi ya Istiqaama katika kata ya Ikwiriri wilayani Rufiji.
 
 Amesema Serikali inaheshimu, inathamini na kutambua mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za kidini katika kujenga jamii ya wacha Mungu na yenye kutii mamlaka na sheria.
 
 Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi zote za kidini zenye nia safi na thabiti,  ili kuhakikisha miradi na mipango mbalimbali ya kijamii na kiroho yenye manufaa kwa umma wa inaendelea kutekelezwa kama ilivyokusudiwa.
 
 Msikiti huo wa Jamiu Assaliheen una uwezo wa kutumiwa na waumini 500 kwa wakati mmoja,  na una vyumba vinne vya madrasa kwa ajili ya kutoa elimu ya dini na malezi mema.