Waziri Mkuu atahadharisha kuhusu corona 

0
190

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Wananchi kujiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima, na wazingatie kukaa umbali wa mita moja au zaidi kutoka mtu mmoja hadi mwingine ili kujikinga na corona.
 
Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo katika Baraza la Eid El Adha lililofanyika kwenye msikiti wa Mtoro, Ilala mkoani Dar es Salaam.
 
Amesema corona ipo nchini, na ni muhimu kwa Wananchi wote wakaendelee kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa huo, ili usiendelee kuenea zaidi.
 
“Tuendeleze tabia ya kunawa mikono mara kwa mara na maji safi yanayotiririka na sabuni,  na tukikosa maji tutumie vitakasa mikono, tuvae barakoa zilizothibitishwa na mamlaka zetu.” Amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa
 
 
Amesema Wananchi wanatakiwa wafanye mazoezi ya mara kwa mara kulingana na afya zao pamoja na mazingira yanayowazunguka, pia amewasihi wazingatie lishe bora.
 
“Kwa wale wenye umri mkubwa na wenye uzito uliopitiliza, na wenye magonjwa sugu kama moyo, pumu, kisukari na figo wanapaswa kuchukua hatua madhubuti zaidi kujikinga na ugonjwa huu.” Amesema Waziri Mkuu

Akizungumzia kuhusu chanjo dhidi ya corona, Waziri Mkuu Majaliwa amesema chanjo hiyo tayari ipo nchini, hivyo Mwananchi yoyote anayetaka kuchanjwa akachanje kwa ajili ya kupata kinga.
 
Hata hivyo, Waziri Mkuu Majaliwa  amewasisitiza Wananchi kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za afya mara waonapo dalili za mafua makali, maumivu ya koo, kichwa kuuma, kupumua kwa shida, kukosa hamu ya kula na kupoteza uwezo wa kunusa harufu mbalimbali.