Waziri Mkuu asitisha likizo za Krismas na mwaka mpya

0
225

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza Makatibu Tawala wa mikoa yote nchini kuhakikisha watendaji wote wa mikoa, wilaya na halmashauri hawaendi likizo ya sikukuu za Krismas na mwaka mpya kwa mwaka huu.

Badala yake viongozi hao wameagizwa wakasimamie ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa na madawati na wawe wamekamilisha ifikapo mwezi februari mwaka 2021.
 
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo jijini Dodoma alipozungumza na Wakuu wa mikoa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI, mkutano uliofanyika kwa njia ya Video.

Kikao hicho kilihusu upokeaji wa taarifa ya maandalizi ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka 2021.

“Suala hili nitalifuatilia mwenyewe ili kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa chaguo la kwanza na la pili wawe wameingia madarasani kufikia Machi Mosi mwaka 2021, ukamilishaji wa vyumba hivyo pamoja na madawati ufanyike kwa kutumia vyanzo vyenu vya ndani vya fedha”, ameagiza Waziri Mkuu.
 
Ameiagiza Ofisi ya Rais TAMISEMI ihakikishe kazi hiyo inakamilika kwa wakati  na amewataka watendaji hao wahakikishe ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa na utengenezaji wa madawati unafanyika usiku na mchana.