Waziri Mkuu asisitiza ulinzi maeneo ya mipakani

0
689

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuongeza ulinzi na doria katika maeneo ya mipaka kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha na vitisho kwa wananchi.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo mkoani Kigoma wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa wilayani Kibondo alipokua akihitimisha ziara yake mkoani humo.

Ameyataja maeneo yaliyo katika hali mbaya  kuwa ni Kibondo, Buhigwe, Kasulu, Ngara, Biharamulo, Uvinza, Kakonko na Kigoma Vijijini  ambako wakazi wake hususani wafanyabiashara wameingiwa na hofu kutokana na kuongezeka kwa vitendo hivyo.

Waziri Mkuu Majaliwa pia ameagiza Wakimbizi wote watakaobainika kutoroka kwenye makambi wanayohifadhiwa na kuingia uraiani wakamatwe na wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria za Tanzania, kwani wanachokifanya ni ukiukwaji wa sheria.

Amesema kuwa pamoja na undugu uliokuwepo baina ya Tanzania na nchi jirani, kila nchi ina sheria na taratibu zake, hivyo ni lazima zifuatwe.

 “Kulinda usalama wa nchi ni jukumu letu sote na si la vyombo vya ulinzi na usalama pekee, kila mmoja anapaswa kushiriki, na kwa upande wa majirani zetu wanaotaka kuja nchini ni lazima wafuate taratibu kwa kuomba vibali,”ameongeza Waziri Mkuu Majaliwa.

Amesisitiza kuwa watu wote wanaoingia nchini  bila ya kufuata sheria na taratibu ndio wanaoshiriki katika vitendo vya uhalifu yakiwemo mauaji ya raia wasiokuwa na hatia, unyang’ani wa kutumia silaha za kivita pamoja na utekaji wa watoto.

Waziri Mkuu ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kulinda mipaka yote nchini,  na watu wote watakaobainika kuingia Tanzania bila vibali wakamatwe na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.