Waziri Mkuu asisitiza Korosho zote zitanunuliwa

0
2211

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahakikishia wakulima wa korosho nchini kuwa korosho zao zote zitanunuliwa.

Akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha korosho cha Terra kilichopo wilayani Kibaha mkoani Pwani akiwa njiani kuelekea mkoani Dodoma,  Waziri Mkuu Majaliwa amesisitiza kuwa serikali kupitia Bodi ya Mazao Mchanganyiko Nchini itanunua korosho zote na hakuna korosho za wakulima ambazo zitabaki bila ya kununuliwa.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, Bodi hiyo ya Mazao Mchanganyiko Nchini  inaendelea kufanya tathmini na kujiridhisha kama kweli korosho hizo zimezalishwa nchini na kuangalia viwango vya ubora.

amesema kuwa hadi sasa zaidi ya Tani  Laki Moja na Elfu Themanini  za korosho  zimekwishakusanywa, na hivyo kuwataka wakulima wa zao hilo nchini waendelee kuiamini serikali kuwa itaendelea kununua korosho zao.

Akiwa katika kiwanda hicho cha korosho cha Terra kilichopo wilayani Kibaha mkoani Pwani, Waziri Mkuu Mkuu Majaliwa  ameupongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kuunga mkono jitihada za serikali za kukuza uchumi kwa kupitia sekta viwanda.

Meneja Utawala wa kiwanda cha Korosho cha Terra, – Peter Ngwale amemweleza Waziri Mkuu kuwa kiwanda hicho kina uwezo wa kubangua Tani  Elfu Sita za korosho kwa mwaka.