Waziri Mkuu Apokea Misaada kukabiliana na CORONA

0
226

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepokea msaada wa fedha pamoja na vitu mbali mbali kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) wenye thamani ya sh. bilioni 1.185 kutoka kwa wadau.

Amewataka Watanzania wote waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo ili kuzuia usisambae zaidi nchini. “Hii ni vita kubwa inahitaji tupigane kwa lengo la kuzuia janga hili lisisambae zaidi nchini, hivyo tuzingatie maagizo ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kumtaka kila Mtanzania ashiriki kwenye vita hii”

Amepokea msaada huo leo katika ofisi ndogo ya Waziri Mkuu iliyoko Magogoni, jijini Dar Es Salaam. Waziri Mkuu amewashukuru wadau hao na kuwataka Watanzania waendelee kushirikiana na Serikali katika hatua zinazochukuliwa kukabiliana na ugonjwa huo.

Miongoni mwa wadau waliotoa msaada huo ni taasisi za kifedha ikiwemo benki ya UBA Tanzania iliyotoa sh. milioni 230, CRDB sh milioni 150 na NMB sh milioni 100. Wadau wengine ni Karimjee Jivanjee Ltd na kampuni zake tanzu waliotoa sh. milioni 200 pamoja na kuahidi kufanyia matengenezo kinga ya magari yote ya Toyota yanayotumika katika kukabiliana na COVID-19 kwa muda ya siku saba bure, Familia ya Karimjee imetoa jenereta la KVA 180 lenye thamani ya sh. milioni 75.

Wengine ni Watoa Huduma ya Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS) ambao wametoa bidhaa mbalimbali zikiwemo magari ya matangazo yatakayotumika kutoa elimu kwa muda wa miezi minne kupitia kampuni ya Advent Construction, maji ya kunywa (Bakhressa Group), Billboard (Ashton Media) vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya sh. milioni 150.

Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) walitoa matanki 1,000 yenye thamani ya sh. milioni 25, huku kila moja likiwa na ujazo wa lita 250, matanki hayo yametengenezwa maalumu kwa ajili ya kunawia mikono, pia Kampuni ya GS1 Tanzania Limited imetoa vitakasa mikono chupa 1,600 zenye thamani ya sh. milioni nne.

Kadhalika, Tanzania Oxygen ltd imetoa msaada wa sh. milioni 158 ambapo wameahidi kufanyia ukarabati kiwanda kikubwa cha kuzalisha oxygen, Mount Meru imetoa vitakasa mikono vyenye thamani ya sh. milioni mbili, Hospitali ya Aga Khan imetoa dawa, sabuni, vitakasa mikono na vifaa tiba vyenye thamani ya sh. milioni 10.220.

Pia, kampuni ya gesi ya Oryx imeahidi kutoa msaada wa kusambaza gesi kwa ajili ya kupikia na matumizi mengine katika hospitali kama kufulia na kwenye vituo vya kuwahifadhi watu wanaohisiwa kuwa pamoja wagonjwa wa COVID-19. Gesi hiyo ina thamani ya sh. milioni 25, Tredea Cosmetics Ltd wametoa vitakasa mikono vyenye thamani ya sh. milioni 1.6.

Umoja wa Mama lishe-Ilala na Machinga wa Kariakoo wametoa sabuni na vitakasa mikono vyenye thamani ya sh. milioni mbili. Wakati huohuo, Chemba ya Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA) wametoa shuka 50, magodoro10, sabuni za maji chupa 170 na vitakasa mikono chupa 400 vyote vikiwa na thamani ya sh milioni tano.

Baada ya kupokea misaada hiyo, Waziri Mkuu kwa niaba ya Rais Dkt. Magufuli aliwashukuru wadau hao kwa vitu mbalimbali walivyovitoa kwa ajili ya kupambana na COVID-19 kwani vifaa pamoja na fedha walizozitoa zitaisadia Serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema Serikali kwa upande wake inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kupambana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha hausambai zaidi nchini. Alitumia fursa hiyo kuwashukuru madaktari, wauguzi pamoja na wataalamu wengine kwa huduma wanazozitoa.

Kuhusu wadau wengine wanaohitaji kutoa misaada, Waziri Mkuu amesema Ofisi yake iko wazi pia wanaweza kupeleka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kwa wanalio nje ya nchi au sehemu yoyote wanaweza kutuma fedha kupitia akaunti yenye Jina la: National Relief Fund Electronic Akaunti Na: 9921159801