Waziri Mkuu aongoza mamia kumuaga Mrema

0
157

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaongoza mamia ya waombolezaji katika misa ya kuuga mwili wa aliyekuwa Mwanasiasa Mkongwe hapa nchini Augustine Mrema.

Misa ya kuuga mwili wa Mrema imefanyika katika kanisa la Mtakatifu Augustino Salasala Mkoani Dar es salaam.

Akitoa salamu za serikali katika ibada hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali itaendelea kumkumbuka Marehemu Mrema kutokana na mchango wake mkubwa wa kuendeleza mahusiano na vyama vya siasa.

“Mheshimiwa Mrema atakumbukwa kama kiongozi mkuu wa Chama cha TLP kwa muda mrefu sana. Na akiwa katika siasa, aliisaidia Serikali kupata mwelekeo mzuri wa vyama vya siasa”-amesema Waziri Mkuu

Kwa upande wake, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu amesema umati mkubwa uliokuwepo kanisani hapo ni ishara tosha ya jinsi Mzee Mrema alivyoishi vizuri na watu wakiwemo viongozi wa Serikali na vyama vya siasa.

Ibada hiyo imeongozwa na Askofu mmoja na mapadre sita. Baadhi ya viongozi waliohudhuria ni Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Mwenyekiti wa chama cha ADC, Hamad Rashid, Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo, Mjumbe wa kamati kuu ya CCM, Steven Wassira,Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na aliyekuwa Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini.