Waziri Mkuu akagua ofisi za Serikali Mtumba

0
431

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua ofisi mpya za wizara Saba katika mji wa Serikali ulioko Mtumba jijini Dodoma.

Akiwa katika mji huo, Waziri Mkuu ameagiza kuwekwa kwa vibao vya ofisi na kukamilishwa kwa mazingira ya nje.

“Kuna wizara hazina majina kwa nje, hakikisheni majengo yote yanawekwa majina haraka ili kuondoa usumbufu kwa wananchi wanaokuja huku kutafuta huduma”, ameagiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Ofisi Saba ambazo Waziri Mkuu Majaliwa amekagua katika mji huo wa serikali wa Mtumba ni ile ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Wizara ya Nishati.

“Nimefurahi kukuta Mawaziri, Naibu wao na Makatibu Wakuu pamoja na wakuu wa idara wako huku na kazi zinaendelea, lakini ni lazima nisisitize kwamba idara zinazohamia huku ziwe ni zile zenye kutoa huduma za kila siku kwa wananchi,” amesema Waziri Mkuu.

Kuhusu miundombinu ya barabara, umeme na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Kamati ya Kitaifa ya kuratibu zoezi la Serikali kuhamia Dodoma inasimamia kazi hiyo ikiwemo suala la ujenzi wa kituo kikubwa cha afya ambacho kitakuwa na huduma zote kwa viongozi lakini pia kitatoa huduma kwa wananchi wanaoishi vijiji vya jirani.