Waziri Mkuu ahitimisha mkutano wa 19 wa Bunge

0
423

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema maambukizi ya virusi corona nchini kwa sasa yamepungua na idadi ya wagonjwa waliopo nchini hadi leo ni 66.

 Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akihitimisha mkutano wa 19 wa bunge na kuongeza kuwa Rais John Magufuli anastahili kupongezwa kwa namna alivyoongoza mapamnao dhidi ya corona.

 “Anayestahili sifa katika hili ni Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa msimamo wake usiotetereka na maono ya mbali aliyokuwa nayo ambayo yamekuwa chachu katika kupunguza maambukizi ya COVID-19 na kulinda uchumi wa nchi,” amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Amesema Tanzania chini ya Rais John Magufuli ilianza kuchukua hatua kadhaa ili kukabiliana na maambukizi ya corona kwa kuunda Kamati tatu za ngazi ya Mawaziri, Watendaji na Wataalam wa afya kwa lengo la kufanya tathmini ya hatua za kuchukua ili kupunguza maambukizi na kulinda anguko la kiuchumi, hatua ambazo zimezaa matunda. 

 Waziri Mkuu amesema suala la kudhibiti maambukizi ya corona litaendelea kuwa kipaumbele cha serikali kwa sasa, pamoja na malengo ya muda mrefu ya kumaliza ugonjwa huo hasa katika kipindi hiki ambacho Shirika la Afya Duniani (WHO) limebainisha kwamba si wa kuondoka mara moja, hivyo  watu wajifunze kuishi nao.