Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa amesema katika uongozi wake hatowasaliti katika kutetea stahiki zao Watumishi wa umma wanaofanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu na uzalendo kwa Taifa lao.
Akizungumza na Viongozi pamoja na Watumishi wa umma wa mkoa wa Kigoma, Waziri Mchengerwa amesema atahakikisha anasimamia haki na stahiki za Watumishi wa umma nchini kwa lengo la kuwaongezea morali ya utendaji kazi kama ambavyo Serikali ya awamu ya sita imekusudia.
Ametoa rai kwa Watumishi wote wa umma nchini kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kuendana na kasi ya Rais Samia Suluhu Hassan, badala ya kufanya kazi kwa mazoea kwani wasipowajibika hatokuwa tayari kutetea stahiki zao.
“Pale ambapo tutabaini kuna mtumishi mzembe, mla rushwa na mbadhirifu wa mali za umma sitokuwa tayari kumtetea lakini nitakuwa tayari kupambana na kumtetea mtumishi yeyote mwadilifu, mchapakazi na mzalendo kwa Taifa lake muda wote asubuhi, mchana, jioni na usiku.” amesisitiza Waziri Mchengerwa