Waziri Mabula awapongeza Wahadzabe kwa kupata hati za ardhi

0
166

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Angeline Mabula ameipongeza jamii ya wawindaji, Wahadzabe, iliyopo wilaya ya Mkalama mkoani Singida kwa utayari iliyouonesha wa kutambua na kukubali kupimiwa maeneo yao na kupatiwa hatimiliki za kimila.

Jumla ya hatimiliki za kimila 100, zikiwemo 26 zinazomilikiwa kwa pamoja kati ya mke na mume, zimetolewa ikiwa ni hatua kubwa kutokana na jamii hiyo kujishughulisha zaidi na uwindaji, utafutaji matunda, urinaji asali na uchimbaji mizizi.

Dkt. Mabula amesema, hatua hiyo inaonesha nia na dhamira njema waliyonayo ya kutaka kuyalinda maeneo yao wenyewe na kwa kushirikiana na serikali.

‘’Hakika hizi ni salamu na ujumbe wa Rais Samia Suluhu Hassan Rais kuwa jamii ya wawindaji inaungana naye na mkoa tayari kwenda naye sambamba katika kuletea watu wote maendeleo,’’ amesema Dkt Mabula.

Wahadzabe ni miongoni mwa jamii ndogo nchini ambazo ziko katika hatari ya kupoteza ardhi wanayoimiliki kutokana na jamii nyingine kuingia na kufanya shughuli zisizoendana na tamaduni za jamii hiyo jambo linalohatarisha ustawi na maisha na desturi za Wahadzabe.