Waziri Jafo awaasa vijana kuuenzi Muungano

0
182

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Selemani Jafo, amewaasa vijana nchini kuendelea kuuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kudumisha amani nchini.

Waziri Jafo ametoa rai hiyo leo wakati akizungumza na TBC, mara baada ya kushiriki Dua maalum ya kumuombea aliyekuwa Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Hayati Sheikh Abeid Amani Karume iliyofanyika katika Ofisi za CCM Kisiwandui huko Zanzibar.

Amesema kuwa vijana wa sasa wanapaswa kuona fahari ya Muungano na kuyaenzi yale yaliyoasisiwa na Hayati Karume ambaye ameacha alama Zanzibar hasa katika ujenzi wa miundombinu na kuwajali Wananchi.

Ameongeza kuwa Hayati Karume alikuwa na maono makubwa kwa Wananchi wake, na mfano wa kuigwa kwa viongozi wengine hapa nchini na Barani Afrika.

“Tukumbuke kwamba Hayati Karume na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere walifanya kazi kubwa ya kuasisi Muungano na leo hii tunajivunia kuwa Watanzania, hivyo kwetu sisi ni faraja hatuna nchi nyingine isipokuwa ni Tanzania,” amesema Waziri Jafo.

Aidha Waziri Jafo amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi kwa uongozi wake ambao umewafanya Wananchi kuwa na imani naye.

Aprili 7 ya kila mwaka ni kumbukumbu ya kifo cha Abeid Amani Karume ambaye alifariki dunia mwaka 1972, na Dua maalum ya kumuombea imefanyika katika Ofisi za CCM Kisiwandui, Zanzibar.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan pamoja na baadhi ya Viongozi mbalimbali, ni miongoni mwa watu walioshiriki katika Dua hiyo.