Waziri Jafo aipa kongole halmashauri ya Buchosa

0
168

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Buchosa mkoani Mwanza kwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa jengo jipya la halmashauri hiyo lenye ghorofa moja pamoja na kituo cha afya cha Isaka.

Waziri Jafo ametoa pongezi hizo alipokagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali katika halmashauri hiyo.

Amesema kwa miradi ya ujenzi wa majengo ya halmashauri pamoja na zahanati inayotekelezwa na Serikali nchi nzima, Buchosa inaongoza kwa kujenga majengo yenye viwango vinavyoendana na thamani ya fedha zilizotolewa.

Aidha, katika ziara hiyo Waziri Jafo amezungumza na Watumishi wa halmashauri hiyo na kuwataka wafanye kazi kwa ushirikiano na kuacha tabia ya kugombana kati ya idara na idara ili kuongeza tija na ufanisi katika kazi zao.

Pia, amemuagiza Mkurugenzi wa halmashauri ya Buchosa kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ili kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa haraka, pamoja na kurahisisha utendaji kazi kwa Watumishi na uendeshaji wa halmashauri hiyo.