Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amewataka Wanajiolojia nchini kuzingatia weledi kwenye taaluma yao, ili iwe na heshima.
“Kuna baadhi ya Wanajiolojia wanawafanya Watanzania waanze kuiona taaluma yenu kuwa haina faida.” amesema Waziri Biteko
Ameyasema hayo mkoani Arusha wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa chama cha Wajiolojia Tanzania (TGS2022).
Pia Waziti Biteko amesema kuna baadhi ya wanajiolojia wamekuwa wakijirahisisha sana na kusababisha hasara kubwa kwa baadhi ya watu na Taifa.
“Taaluma hii imesababisha hasara kwa watu wengi kwa sababu ya watu wachache wasiokuwa waaminifu.” amesema Dkt. Biteko
Vilevile Waziri Biteko amethibitisha kuwa migogoro mingi kwenye sekta ya madini hasa kwenye leseni chanzo chake ni wajiolojia kuchukua fedha na kuuza taarifa bila uaminifu.
“Tuambiane ukweli watu wanavamia maeneo chanzo mjiolojia mmoja, mnatumia mpaka wachimbaji wadogo, naomba sana ifanyeni taaluma iwe inaaminika.” amesema Waziri Biteko
Pia amewataka wanachama wa Jumuiya ya Wanajiolojia kujisimamia vizuri, ili taaluma hiyo iwe na heshima.
“Mmeruhusu makanjanja kuwa na sauti kuliko nyie wenye taaluma halisi, wako watu wengi wamelizwa na watu wanaojiita wanajiolojia kutokana na kupenda taarifa feki.” amesema Waziri Biteko
Amewahakikishia Wanajiolojia nchini uwepo wa mchakato wa kuundwa kwa Bodi ya Wanajiolojia.
“Natamani nione nchi hii wanaosimamia ni Majiolojia na si Majolo, majolo wana nguvu na sauti kubwa kuliko wanajiolojia, wanaeleza utajiri ambao haupo, kazi yao ni kuandika meseji, majolo kazi yao nikudili na mitandao washindeni majolo kwa kuonesha ujiolojia unalipa kuliko ujolo.” amesisitiza Waziri Biteko