Waziri Bashungwa : Tunataka Ethiopia waisome namba mchezo kati yao na Tanzanite

0
187

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa ameliagiza Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kushirikiana na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuhakikisha wanaiwekea mazingira wezeshi timu ya Taifa ya Wanawake chini ya umri wa miaka 20 (Tanzanite) yatakayoijenga kimwili na kisaikolojia katika kuikabili timu ya Taifa ya Ethiopia mwezi Januari mwaka 2022.

Waziri Bashungwa ametoa agizo hilo alipokutana na Wachezaji pamoja na kamati ya ufundi ya timu hiyo kwa lengo la kujadili changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakiwa nchini Burundi, wakati wa mchezo baina ya Tanzanite na timu ya Wanawake ya Burundi ya chini ya umri wa miaka 20.

Amesema kazi ya Serikali katika sekta ya michezo ni kuweka mazingira wezeshi kwa wanamichezo na timu zote zinazoipeperusha bendera ya Taifa, na ndoto ya Serikali ni kuwaona wachezaji na timu zao wakiibuka washindi katika michezo yote.

Waziri Bashungwa pia ameipongeza timu ya Tanzanite kwa mchezo wao dhidi ya Burundi uliochezwa tarehe 18 mwezi huu, ambapo iliibuka na sare ya bao moja licha ya kucheza wakiwa pungufu.

“Kwa kweli mliishangaza Afrika na dunia huko Burundi, yaani mnacheza pungufu lakini bado tukapata ushindi wa heshima, kwa kweli tunawapongeza sana vijana wetu.” amesema Waziri Bashungwa

Timu ya Taifa ya Wanawake chini ya umri wa miaka 20 inashiriki michezo hiyo ambayo ni ya awali ili kupata tiketi ya kufuzu kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia yanayotarajiwa kufanyika mwaka 2022 nchini Costa Rica.