Waziri Bashungwa awafariji Stars

0
216

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amekutana na wachezaji pamoja na benchi la ufundi la timu ya taifa ya mpira wa miguu (Taifa Stars) na kuwaeleza kuwa Taifa linawaamini na bado wana nafasi kubwa ya kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia vipaji vyao katika soka licha ya kupoteza mchezo dhidi ya timu ya taifa ya DRC.

Waziri Bashungwa ameyasema hayo leo Novemba 12, 2021, katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, alipokutana na ujumbe wa timu hiyo kabla ya kuanza safari kuelekea nchini Madagascar kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo, utakaochezwa siku ya jumapili Novemba 14, 2021.

Amesema licha ya kupoteza mchezo dhidi ya timu ya taifa ya DRC, lakini watanzania wanatamani kusikia timu yao ikifanya vizuri katika mchezo wao dhidi ya timu ya Madagascar.

“Ni kweli tumefungwa na DRC lakini Mchezo kati ya Taifa Stars na Madagascar ni wa muhimu sana kwetu kama taifa na kwa FIFA hasa katika kupanga madaraja ya timu zilizo bora duniani” amesema Waziri Bashungwa.

Kwa upande wake meneja wa Taifa Stars Nadir Haroub ‘Canavaro’ amesema wana imani ya kufanya vizuri katika mchezo huo, huku akiomba Watanzania kuendelea kuwa na imani na timu yao na kuiombea ili ifanye vizuri katika mchezo huo.