Waziri wa Maji Jumaa Aweso, ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa jitihada kubwa walizozifanya wakati wa changamoto ya upungufu wa maji Mkoani Dar es Salaam huku akiwataka kuharakisha mradi wa Kidunda na Rufiji.
Aweso ameyasema hayo leo alipokutana na Menejimenti ya Dawasa na kuwataka kuharakisha mchakato wa miradi hiyo ili adha ya maji katika jiji la Dar es Salaam isijirudie tena ikiwa ni pamoja na mradi wa Maji Kigamboni.
Mapema mwezi Novemba, mkoa wa Dar es Salaam ulikumbwa na adha kubwa ya uhaba wa maji na kupelekea kuwa na mgao kitendo ambacho kilimlazimu Aweso kutinga ofisi za Dawasa usiku wa Novemba 17 na kuwataka wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kufanya kazi usiku na mchana ili mfumo wa ugawaji maji urejee katika hali yake ya kawaida.
“Nina kila sababu ya kuwashukuru na kuwapongeza kwa jitihada kubwa ambazo mlizifanya kipindi cha changamoto ya maji, mlifanya kazi usiku na mchana na kuhakikisha hali ya maji inarejea, naomba changamoto hii isijirudie tena, harakisheni miradi ya Kidunda na Rufiji ili adha iliyojitokeza isijirudie” amesema Aweso.
Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema, utafiti wa mradi wa Bwawa la Kidunda umekamilika na ule wa Rufiji upo mbioni kuanza.
“Mradi wa Rufiji utakamilika na malengo yetu ukamilike kabla ya mwaka 2025 ili uzinduliwe na Rais Samia(Samia Suluhu Hassan),” amesema Luhemeja