Waziri ataka maboresho ya mawasiliano mpakani

0
224

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye ametembelea kijiji cha Kirongwe kilichopo wilaya ya Rorya mkoani Mara na kukagua huduma za mawasiliano katika eneo hilo.

Wakati wa ziara yake Waziri Nape amekagua mnara wa mawasiliano wa kampuni ya Halotel ambao umekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha huduma za mawasiliano katika eneo hilo la mpakani.

Pia ametembelea eneo la Muhuru Bay, mpakani mwa Tanzania na Kenya na kuzungumza na watendaji wa ofisi za uhamiaji upande wa Tanzania na Kenya.

Waziri Nape amesema kumekuwa na changamoto ya kukosekana kwa huduma bora za mawasiliano katika maeneo ya mpakani, na mara nyingi wananchi wamekuwa wakitumia huduma za mawasiliano za nchi jirani.

Kufuatia hali hiyo Waziri Nape ameliagiza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuhakikisha linafikisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika eneo la mpaka huo ili kuongeza nguvu ya mawasiliano.

Jumla ya minara 758 inajengwa nchini kote ili kuboresha huduma za mawasiliano vijijini, ambapo wilaya ya Rorya imepata minara 10.