Rais Samia Suluhu Hassan ameruhusu Mzee Hashim Msuya na mkewe wake waliofiwa na watoto wanne katika ajali ya gari iliyotokea Chalinze mkoani Pwani Agosti 02, 2023 kutibiwa bure katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Akitoa taarifa hiyo kwa niaba ya Rais, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amesema, baada ya kuongea na Rais ameridhia wazazi hao wapate matibabu bure endapo wataugua katika hospitali hizo.
“Rais alijua tunaaga jana, lakini kutokana na ratiba kumbana leo yupo Mbeya na ameniagiza nifikishe salamu za pole kwa familia. Pia ameniagiza kuwa wazee hawa endapo wataugua basi wapate matibabu bure katika hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na hili ameniambia nimfikishie Profesa Janabi na Dkt. Kisenge wa JKCI.” amesema Chalamila.
Katika hatua nyingine Chalamila amewasihi ndugu kutoa msaada kwa familia, kwani waliokuwa wanategemewa wametangulia mbele ya haki.
“Familia imepoteza watoto wanne ambao walikuwa tegemezi, hapa wengine wanalia kwa sababu wanaona hakuna atakayeweza kuwasaidia tena kwa hiyo hili lisiishie hapa tu tuwasaidie hawa ndugu kadri tuwezavyo.” ameongeza Chalamila.