Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam,v Amos Makalla ametoa muda wa mwezi mmoja kwa wavamizi wa ardhi ya kiwanda cha Wazo, kuhakikisha wanapokea ankara na kuanza malipo ya fidia kwa mujibu wa makubaliano yaliyokuwa yamewekwa awali.
Makalla ametoa maelekezo hayo wakati wa kupokea taarifa ya mwenendo wa zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi wa Chasimba, Chatembo na Chachui, ambapo amesema endapo wananchi watakaidi agizo hilo serikali itajitoa rasmi katika kuwadhamini na kuachia kiwanda kutekeleza amri ya mahakama ambayo ni kuwabomolea makazi yao.
Amesema taarifa inaonyesha kati ya wavamizi wote 4,070, ni wavamizi 39 tu wamelipa na wanastahili hati, 150 wamelipa ada ya kuomba kupata hati na 3,881 wamekaidi kulipa.
Kuhusu wavamizi wapya waliovamia eneo la kiwanda na eneo la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam amemuelekeza mkuu wa wilaya ya Kinondoni kuhakikisha wavamizi hao wanaondolewa mara moja.
Makalla pia amewashauri wavamizi hao kujiadhari na wanasiasa wanaotumia zoezi hilo kama mtaji wa kisiasa, kwa kuwa jambo hilo limekaa kisheria.
Wananchi 4,070 walivamia eneo la kiwanda cha Wazo ambacho ni mmiliki halali wa eneo hilo na mahakama ilitoa amri ya kuondolewa kwa wananchi hao baada ya kushindwa kesi.
Jambo hilo liliwalazimu waiombe serikali iwasaidie kutafuta muafaka na baada ya mazungumzo baina ya serikali na kiwanda, iliamuriwa walipe shilingi 6,419 kwa mita za mraba badala ya shilingi elfu 40 iliyopendekezwa na kiwanda.
Hata hivyo wananchi hao wamekaidi kulipa fidia hiyo.