Watumishi wa Umma wasisitizwa kuwasilisha TIN namba

0
375

Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi Rasilimali Watu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ibrahim Mahumi amewasihi Watumishi wa Umma ambao hawajawasilisha namba za utambulisho wa mlipakodi (TIN) kufanya hivyo.

Akizungumza jijini Dar es salaam katika Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Mahumi amewatoa hofu Watumishi wa umma kwa kuwaeleza kuwa TIN hizo hazitotumiwa kuongeza makato kwenye mishahara yao bali zinatumika kwenye masuala ya utawala.

Kuhusu kutambua umri wa kustaafu wa Watumishi wa umma ameeleza kuwa, Serikali itaoanisha taarifa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ofisini kwa mtumishi pamoja na shule alizosoma.

Baada ya kukusanya taarifa zote, Mahumi amesema ile itakayoonesha umri wa mapema zaidi wa mtumishi kustaafu, ndiyo itakayotambulika kama tarehe yake halali ya kuzaliwa.

Amebainisha kuwa hatua hiyo imetokana na kuwepo kwa udanganyifu kuhusu tarehe za kuzaliwa kwa Watumishi wengi, na hivyo wengine kuendelea kuwepo kwenye utumishi licha ya kufikisha umri wa kustaafu.