Watumishi sita wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu – HESLB waachishwa kazi.

0
1954

Wakurugenzi watano na Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Hesabu wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu – HESLB wameachishwa kazi baada ya kubainika kuhusika na makosa mbalimbali ikiwemo kushindwa kutekeleza majukumu yao na uzembe hali iliyoisababishia serikali hasara.

Katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul –Razaq Badru amesema maamuzi hayo yamefikiwa na Bodi ya wakurugenzi wa Bodi ya Mikopo.

Walioachishwa kazi ni Juma Chagonja aliyekuwa Mkurugenzi wa Urejeshaji wa Mikopo, Onesmus Laizer aliyekuwa Mkurugenzi wa Upangaji na Ugawaji Mikopo, John Elias aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Ugawaji Mikopo, Robert Kibona aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Urejeshaji Mikopo, Heri Sago aliyekuwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Hesabu na Chikira Jahari aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Upangaji Mikopo.

Mwaka 2016 na 2017 Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya mikopo ya Elimu ya Juu iliwasimamisha kazi Wakurugenzi WATANO na Mkaguzi Mkuu wa ndani wa hesabu wa bodi hiyo ya mikopo.

Mapema mwaka huu HESLB iliunda kamati kuwachunguza watumishi hao na matokeo ya kamati hiyo yamewatia hatiani.

Kwa upande wake Mwanasheria wa Bodi hiyo Abdul Mtibora amesema rufaa iko wazi endapo hawajaridhika na uamuzi wa bodi ya wakurugenzi.

 

Ngarayai Kimosa

13 Juni 2018