Watumishi 22 wa TRA kusimamishwa kazi

0
288

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Philip Mpango ameagiza kusimamishwa kazi kwa watumishi 22 wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazowakabili.

Dkt Mpango ametoa agizo hilo jijini Dodoma katika kikao kilichozihusisha bodi za Wakurugenzi, Menejimenti na Mameneja wa mikoa wa mamlaka hiyo.

Amesema watumishi hao wameshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kujihusisha na ufisadi na kuikosesha mapato serikali.

Amebainisha kuwa wafanyakazi hao wanatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa, kutosimamia ipasavyo matumizi ya mashine za kutolea stakabadhi (EFD’s) na kuwabambikia kodi kubwa wafanyabiashara.

Dkt Mpango ametaka kupatiwa taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo ndani ya kipindi cha siku 90 kuanzia leo Desemba 16, 2020.