Watumiaji wa intaneti waongezeka kwa 6.7 %

0
649

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema kuna ongezeko la asilimia 3.4 ya laini za simu, huku matumizi ya huduma za intaneti, mitandao ya kijamii na huduma za kifedha kwa mtandao nayo yakiongezeka.

Matumizi ya huduma huduma za kifedha kwa mtandao yameongezeka kutoka miamala ya shilingi bilioni 349.9 hadi shilingi bilioni 366.1 kufikia mwezi Septemba mwaka huu.

Ripoti ya utendaji ya sekta ya mawasiliano kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2022/2023, iliyotolewa na TCRA imeonesha kuwa idadi ya laini za simu zinazotumika hadi kufikia mwezi Septemba mwaka huu ni milioni 58.1 kutoka milioni 56.2 mwezi Juni mwaka huu.

Takwimu zinaonesha kuwa mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha , Mbeya na Tabora inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya laini zinazotumiwa na watu na zinazotumika kwa ajili ya mawasiliano kwa mashine.

Akitoa ripoti hiyo mkoani lDar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Bakari amesema, kuna ushindani mkubwa kati ya watoa huduma, kwani hakuna mtoa huduma mwenye zaidi ya asilimia 35 ya laini zilizosajiliwa.

Amesema kuwa watumiaji wa intaneti wameongezeka kutoka milioni 29.1 mwezi Juni mwaka huu hadi milioni 31.1 mwezi Septemba mwaka huu sawa na ongezeko la asilimia 6.7.