Watuhumiwa wa utoroshaji dhahabu kortini

0
468

Kesi ya uhujumu uchumi namba Tatu ya mwaka 2019 inayowakabili watuhumiwa 12 wakiwemo Wafanyabiashara wa madini ya dhahabu pamoja na maafisa wa polisi imetajwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza.

Watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wakikabiliwa na mashtaka 12, ikiwa ni pamoja na uhujumu uchumi, kujihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa, kutakatisha fedha zaidi ya Shilingi Milioni Mia Tatu na kuisababishia serikali hasara ya Shilingi Bilioni 1.8.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Gwae Sumaye, Wakili wa Serikali Castus Ndamgoba amesema kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa tena.

 Watuhumiwa hao wanatetewa na mawakili Wanne wakiongozwa na Steven Makwega ambaye ameomba kufuatwa kwa kalenda ya mahakama kutokana na Jamhuri kushindwa kuwafikisha watuhumiwa hao mahakamani Februari 25 mwaka huu kwa madai ya mvua kunyesha.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Sumaye ametaka kuwepo mawasiliano baina ya Wakili wa Serikali na Mawakili wanaowatetea watuhumiwa hao ili kuondoa sintofahamu iliyotokana na kesi hiyo kutotajwa februari 25 mwaka huu.

Inadaiwa kuwa Januari Nne mwaka huu watuhumiwa Sajid Abdalah, Kisabo Nkinda, Emmanuel Kija na Hassa Sadick waliwapatia watuhumiwa Wanane ambao ni askari polisi rushwa ya Shilingi Milioni Mia Saba ili kuwasaidia kutorosha Kilo 319 za dhahabu zenye thamani ya Shilingi Bilioni 27.

Watuhumiwa wote 12 hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Mwanza haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi.

Watuhumiwa  wote wamerejeshwa mahabusu na kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 27 mwaka huu itakapotajwa tena.