Watu watano wafariki kwa kuangukiwa na Ghorofa Moshi

0
155

Watu watano wamefariki dunia na wengine tisa kujeruhiwa baada ya kuangukiwa na kifusi kwenye gorofa walilokuwa wakilijenga katika kijiji cha Sembeti Marangu wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.

Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Abbas Kayanda amesema tukio hilo limetokea jana majira ya saa tatu usiku ambapo kulikuwa na wafanyakazi 30, na 16 kati yao walisalimika wakati jengo hilo linaanguka.

Kayanda amesema serikali itaunda timu ya kuchunguza sababu za kuanguka kwa jengo hilo na kusababisha vifo vya watu hao na kwamba miili ya marehemu iko Hospitali ya Marangu.

Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Jeremiah Mkomagi amesema kwa sasa wanaendelea na zoezi la kuchimbua kifusi zaidi kuangalia kama kuna uwepo wa mtu mwingine.

“Kazi ya kuendelea kukata zile nondo ambazo zilianguka na kile kifusi pamoja na kutoa matofali na kifusi cha mchanga ili kuangalia kama kuna majeruhi wengine ama miili ya watu wengine ambao waliingia bila kujulisha wasimamizi,” alisema

Mhandisi Mkomagi amesema jengo hilo ni la ghorofa mbili ambapo ujenzi wake ulikuwa ukiendelea na kwamba ni wiki tatu tangu ujenzi uanze.