Watu tisa wamefariki dunia na wengine wameugua baada ya kuvuja kwa hewa ya sumu kutoka katika kiwanda kimoja kwenye Mji wa Visakhapatnam katika Jimbo la Andhra Pradesh, Kusini mwa India.
Taarifa zinaeleza kuwa mamia ya watu wamekimbizwa hospitali kufuatia kuvuta hewa hiyo ya sumu huku wakilalamika kupata maumivu makali machoni na kupumua kwa taabu.
Mamia ya wananchi wanaoishi jirani na kiwanda hicho wanaendelea kuhamishiwa katika maeneo yenye usalama.
Afisa kutoka Mamlaka ya Kudhibiti Uchafuzi wa Mazingira katika jimbo hilo, Rajendara Reddy amesema gesi iliyovuja ni Styrene na kwamba kiwanda kilichohusika kilikuwa kikifunguliwa kwa mara ya kwanza tangu kufungwa Machi 24 mwaka huu kufuatia kuzuka kwa janga la corona.