Watu bilioni moja kutazama filamu ya The Royal Tour

0
285

Katibu Mkuu wa wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya utengenezaji wa filamu ya The Royal Tour Dkt Hassan Abbasi amesema kwa kipindi kifupi filamu hiyo inatarijiwa kutazamwa na watu zaidi ya bilioni moja duniani.

Dkt Abass amesema hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuelekea uzinduzi wa filamu hiyo visiwani Zanzibar na kueleza kuwa filamu hiyo imeshaanza kuleta faida kubwa tangu ilipozinduliwa nchini Marekani.

Kwa hapa nchini, tayari filamu ya The Royal Tour imezinduliwa jijini Arusha na kesho itazinduliwa Zanzibar na inatarajiwa kuzinduliwa kitaifa jijini Dar es Salaam tarehe 8 mwezi huu.

Ameeleza kuwa filamu ya The Royal Tour imekuwa na mafanikio makubwa kwa muda mfupi tangu kuzinduliwa ambapo matajiri na wafanyabiashara wakubwa wa Marekani wameonesha nia ya kuwekeza Tanzania Katika sekta mbalimbali.

“Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa kuitangaza Tanzania akishirikiana kwa ukaribu na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi katika kuifanya filamu hiyo kuwa ya kipekee na kuvutia watu wengi duniani.

Aidha amesema kuwa lengo la kushirikiana na waandaji wa kimataifa kufanya filamu hiyo ilikuwa ni kutaka kuwafikia watu wengi zaidi duniani na wazoefu Katika Kazi hizo na kueleza kuwa haki miliki za filamu hiyo zipo vizuri.

Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi, Tanzania itanufaika zaidi kutokana na kuzalisha filamu hiyo ambayo wadau mbalimbali ndio wamechangia kugharamia maandalizi, bila kutumia pesa kutoka Serikalini.