Watu 20 wamefariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa mkoani Kilimanjaro kwa kukanyagana wakati wakigombea mafuta ya upako yaliyokuwa yakitolewa katika mkutano wa Mtume Boniface Mwamposa uliofanyika katika Uwanja wa Majengo mjini Moshi.
Ajali hiyo imetokea Februari Mosi mwaka huu ambapo mbali na hao waliofariki wengine waliojeruhiwa wamepelekwa sehemu mbalimbali kupatiwa matibabu zikiwamo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawezi, Hospitali ya Rufaa ya KCMC.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba amethibitisha kutokea kwa vifo vya waumini hao, huku hofu ikizidi kutanda kwamba huenda vifo hivyo vikaongezeka kutokana na waliojeruhiwa.
Jeshi la Polisi mkoani humo limemtaka Mwamposa kujisalimisha kwa ajili ya mahojiano kutokana na vifo hivyo. Aidha, jeshi hilo limekiri kuwa linawashikilia watu saba akiwamo mchungaji wa Kanisa la Calvary Assemblies of God, Elia Mwambapa kwa mahojiano.
Akieleza sababu ya mchungaji huyo kukamatwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Salum Hamduni amesema mchungaji huyo ndiye aliyeomba kibali cha kongamano hilo la siku tatu lililomalizika jana Jumamosi.
Waumini katika mkutano huo walikuwa wakigombea kukanyaga mafuta yaliyomwagwa na Mwamposa kwa madai kuwa yalikuwa na upako.
Kati ya watu hao waliofariki watoto ni wanne (wawili wa kiume na wawili wa kike) na watu wazima ni 16 (15 ni wanawake).