Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Batilda Burian amewataka wazazi wa kijiji cha Msomera Wilaya ya Handeni kuwapeleka watoto shule na sio kuwapangia majukumu ya kuchunga ng’ombe wakati umri wao ni wa kwenda shule kusoma.
Dkt. Batilda amesema hayo baada ya kuwatembelea wananchi waliohamia kwa hiari katika kijiji cha Msomera wakitokea eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.
Amewataka wazazi kuwapa haki ya msingi watoto kwa kuwapeleka shule pale tu umri wao wa kuanza shule unapofika kwani hilo ni Taifa la kesho na ni faida kwa wazazi na watoto pia.
Aidha, Dkt. Batilda amesema katika sekta ya Afya amemuelekeza mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando kutafuta na kumpatia nyumba Daktari mkuu ili aweze kuishi karibu na kituo cha afya kilichopo katika kijiji hicho na huduma ya afya iweze kupatikana muda wote.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Tanga ameongezea kuwa Serikali itaendelea kuzishughulikia changamoto za wananchi wa kijiji hicho cha Msomera na kuendelea kuwapatia huduma bora.