Watoto waliofaulu Mkoani Dodoma marufuku kusafiri bila kibali

0
851

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge amepiga marufuku wazazi kuwasafirisha watoto waliomaliza elimu ya msingi na kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kutoka nje ya mkoa pasipo kibali cha uongozi wa kijiji ili kuhakikisha watoto wote waliofaulu wanajiunga na Kidato cha kwanza.

Dokta Mahenge ametoa onyo hilo katika ziara ya kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa Wilayani Chamwino ili kuwawezesha wanafunzi wote waliofaulu wanapata nafasi ya kujiunga na elimu ya sekondari ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.

Dokta Mahenge pia amezitaka halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma  kuweka mikakati ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa wanafunzi watakaochaguliwa mwaka ujao wa 2020, badala ya kusubiri matokeo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga amesema wanakabiliwa na changamoto ya kuwaandikisha wanafunzi ambao wanatoka kwenye familia za wavuvi na wafugaji kutokana na kuhamahama.