Watanzania watakiwa kutovamia hifadhi ya barabara

0
788
Rais John  Magufuli ameweka jiwe la msingi la upanuzi wa barabara ya Morogoro iliyopo  jijini Dar es salaam katika eneo la  kuanzia Kimara mkoani Dar es salaam hadi Kibaha mkoani Pwani yenye urefu wa Kilometa 19.2.
Upanuzi huo utahusisha kuongeza njia za kupita magari kutoka mbili zilizopo sasa hadi nane, kujenga madaraja sita na makalavati 36 na kujenga barabara ya juu katika eneo la Kibamba CCM kwenye makutano ya barabara inayotokea Bunju na barabara ya kwenda hospitali ya Mloganzila.
Sherehe hizo za kuweka jiwe la msingi la upanuzi huo zimefanyika katika eneo la Kimara Stop Over na kuhudhuriwa na Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai, Mawaziri, Wabunge, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa mkoa wa Dar es salaam wakiongozwa na Mkuu wa mkoa huo Paul Makonda.
Akizungumza wakati wa sherehe  hiyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema kuwa barabara ya Morogoro ni lango kuu la usafiri kati ya jiji la Dar es salaam lenye bandari kuu na mikoa mingi ya Tanzania Bara na nchi jirani na kwamba upanuzi wake utasaidia kupunguza msongamano mkubwa wa magari takribani elfu  50 yanayopita katika barabara hiyo kila siku.
Mhandisi Mfugale ameongeza kuwa, upanuzi wa barabara hiyo pia utaokoa muda kutoka saa tatu zinazotumika kupita eneo hilo kwa sasa hadi nusu saa.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mfugale, upanuzi wa barabara hiyo ya Morogoro kuanzia eneo la Kimara hadi Kibaha,  utafanyika kwa muda wa miezi 30 kuanzia Julai 21 mwaka huu wa 2018 kwa gharama ya shilingi Bilioni 141.56, fedha zinazotolewa na serikali.
Akizungumza katika sherehe hizo,  Rais Magufuli amewapongeza wakazi wa mkoa wa Dar es salaam kwa kupatiwa mradi huo mkubwa na kubainisha kuwa pamoja na barabara hiyo, serikali  inaendelea kuboresha miundombinu ya Dar es salaam ambapo barabara zenye jumla ya kilometa 212 zinajengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 660.
Kuhusu fidia kwa nyumba zilizovunjwa wakati wa upanuzi wa barabara hiyo, Rais Magufuli amewataka wanasiasa kuacha kuwapotosha wananchi kuwa watalipwa fidia.
Amesisitiza kuwa serikali haitalipa fidia kwa mtu yeyote aliyejenga katika eneo la hifadhi ya barabara kwa mujibu wa sheria.
“Kuna wanasiasa wanataka waonekane wao ndio wanawatetea wananchi na wanasema serikali itoe fidia, nataka niwaambie ndugu ukivamia barabara unatafuta umasikini, fidia haipo, fidia haipo, narudia fidia haipo” amesisitiza Rais Magufuli.
 Amewataka  Watanzania kote nchini kuacha kuvamia maeneo ya hifadhi ya barabara na kujenga makazi.
Naye Spika wa Bunge Job Ndugai amempongeza Rais Magufuli kwa namna serikali inavyosimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo na kumhakikishia kuwa Bunge litaendelea kuunga mkono juhudi hizo zenye maslahi kwa Taifa.