Watanzania watakiwa kutokwenda China kwa sasa

0
277

Balozi wa Tanzania nchini China Mbelwa Kairuki amewataka Watanzania hasa Wanafunzi wenye viza na hati za ukazi za kuishi nchini China, kutorejea katika nchi hiyo mpaka hapo watakapojulishwa.

Balozi Kairuki ametoa kauli hiyo kufuatia serikali ya China kutangaza kusitisha kupokea raia wa kigeni kuanzia machi 28 mwaka huu hata kwa wale wenye viza na hati za ukazi, lengo likiwa ni kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vya corona.

Amewataka Watanzania wote kuheshimu tangazo hilo la serikali ya China, kwa kuwa suala hilo ni la muda mfupi na hali itakaporejea kama kawaida wataruhusiwa kuingia tena nchini humo.

Balozi huyo wa Tanzania nchini China amesisitiza kuwa, Watanzania wote waliopo nchini China wako salama na kwamba maambukizi ya corona nchini humo yameendelea kupungua kwa kiwango kikubwa.

Amesema kwa siku tatu mfululizo, China haina kabisa maambukizi mapya ya corona, na kwamba hata katika mji wa Wuhan uliopo kwenye jimbo la Hubei ambako virusi hivyo vilianzia , wakazi wake wameruhusiwa kutoka nje ya mji huo.

Kwa mujibu wa Balozi Kairuki, treni ya kwanza yenye abiria takribani mia nane imeruhusiwa kusafiri kutoka kwenye jimbo la Hubei kwenda Beijing.