Watanzania watakiwa kufanya kazi kwa bidii

0
1869

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako ametoa wito kwa Watanzania kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Profesa Ndalichako ametoa wito huo jijini Dar es salaam wakati wa kongamano la kumbukizi ya miaka 19 ya kifo cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

Profesa Ndalichako ameongeza kuwa kupitia kongamano hilo ni vema elimu kuhusu uzalendo na uadilifu ikatolewa, kwa kuwa mipango ya taifa kuwa na uchumi wa viwanda haitafanikiwa bila kuwa na vijana waadilifu.

Akichangia mada kuhusu umuhimu wa Azimio la Arusha katika kustawisha viwanda, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt Ayub Rioba amesema kuwa miongoni mwa malengo yaliyowekewa msisitizo zaidi katika azimio la Arusha ni kufanya kazi kwa bidii.