Watanzania watakiwa kudumisha maadili mema

0
471

Mufti wa Tanzania, – Sheikh Abubakar Zubeir amewataka waumini wa dini ya Kiislam nchini na Watanzania wote kudumisha maadili mema yanayompendeza Mwenyezi Mungu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Mufti amesema kuwa hakuna dini yoyote duniani inayoruhusu vitendo vya mmomonyoko wa maadili, hivyo ni vema jamii ikatenda matendo mema na kuwalea watoto katika maadili ya kupendeza.

Akizungumzia sherehe za Maulid za kuzaliwa kwa Mtume Muhammad, Mufti wa Tanzania amesema kuwa sherehe hizo kitaifa zitafanyika wilayani Korogwe mkoani Tanga Novemba 19 mwaka huu na Baraza la Maulid litasomwa tarehe ishirini mwezi huu.

Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir pia ametumia mkutano wake na waandishi wa habari, kuzungumzia maadhimisho ya miaka hamsini ya Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA), maadhimisho yatakayofikia kilele chake Disemba 17 mwaka huu na kuwataka waumini wa dini ya kiislam nchini kujitokeza na kushiriki katika maadhimisho hayo.